2 Chronicles 21

Yehoramu Atawala

(2 Wafalme 8:17-24)

1 aYehoshafati akalala na baba zake, akazikwa pamoja nao katika Mji wa Daudi. Mwanawe Yehoramu akawa mfalme baada yake. 2Ndugu zake Yehoramu, wana wa Yehoshafati walikuwa: Azaria, Yehieli, Zekaria, Azaria, Mikaeli na Shefatia. Hawa wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli
Yaani Yuda.
3 cBaba yao alikuwa amewapa zawadi nyingi za fedha na dhahabu na vitu vya thamani, pamoja na miji yenye ngome huko Yuda, bali ufalme akampa Yehoramu kwa sababu alikuwa mwanawe mzaliwa wa kwanza.

4 dBaada ya Yehoramu kujiimarisha katika ufalme wa baba yake, akawaua kwa upanga ndugu zake wote pamoja na baadhi ya wakuu wa Israeli. 5Yehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka minane. 6 eAkaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alimwoa binti wa Ahabu. Akatenda maovu machoni pa Bwana. 7 fHata hivyo, kwa sababu ya Agano ambalo Bwana alikuwa amefanya na Daudi, Bwana hakuwa radhi kuangamiza nyumba ya Daudi. Mungu alikuwa ameahidi kuidumisha taa kwa ajili yake na wazao wake milele.

8 gWakati wa Yehoramu, Edomu waliasi dhidi ya Yuda na kujiwekea mfalme wao wenyewe. 9Basi Yehoramu akaenda huko pamoja na maafisa wake na magari yake ya vita. Waedomu wakamzunguka yeye na majemadari wake wa magari yake ya vita, lakini akaondoka, akapenya usiku na kuwashambulia Waedomu. 10 hHadi leo Edomu wameasi dhidi ya Yuda.

Libna pia wakaasi wakati huo huo kwa sababu Yehoramu alikuwa amemwacha Bwana, Mungu wa baba zake.
11 iAlikuwa pia ametengeneza mahali pa juu pa kuabudia miungu katika vilima vya Yuda na akawa amewasababisha watu wa Yerusalemu kufanya uzinzi na akawa amewapotosha watu wa Yuda.

12 j kYehoramu akapokea barua kutoka kwa nabii Ilya iliyosema:

“Hili ndilo Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asemalo: ‘Hukuenenda katika njia za Yehoshafati baba yako au za Asa mfalme wa Yuda.
13 lLakini umeenenda katika njia za wafalme wa Israeli, nawe umewaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu kuzini, kama vile nyumba ya Ahabu ilivyofanya. Pia umewaua ndugu zako mwenyewe, watu wa nyumbani mwa baba yako, watu waliokuwa bora kuliko wewe. 14Hivyo basi Bwana yu karibu kuwapiga watu wako, wanao, wake zako na kila kitu kilicho chako, kwa pigo zito. 15 mWewe mwenyewe utaugua sana kwa ugonjwa wa tumbo kwa muda mrefu, hadi ugonjwa utakaposababisha matumbo yako kutoka nje.’ ”

16 n Bwana akaamsha chuki ya Wafilisti na ya Waarabu walioishi karibu na Wakushi dhidi ya Yehoramu. 17 oWakaishambulia Yuda, wakaivamia na kuchukua mali zote zilizopatikana katika jumba la mfalme pamoja na wanawe na wake zake. Hakubakiziwa mwana yeyote isipokuwa Ahazia aliyekuwa mdogo wa wote.

18Baada ya mambo haya yote, Bwana akampiga Yehoramu kwa ugonjwa usioponyeka wa matumbo. 19 pIkawa baada ya muda, mwisho wa mwaka wa pili, matumbo yake yakatoka nje kwa sababu ya ugonjwa, naye akafa katika maumivu makali sana. Watu wake hawakuwasha moto kwa heshima yake, kama walivyokuwa wamewafanyia baba zake.

20 qYehoramu alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipokuwa mfalme, naye akatawala huko Yerusalemu miaka minane. Akafa, bila kusikitikiwa na mtu yeyote, naye akazikwa katika Mji wa Daudi, lakini si katika makaburi ya wafalme.
Copyright information for SwhKC